Taswira ya CCM haitarejea kwa staili ya Kikwete Mwandishi wetu |
FEBRUARI 5 mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilisherehekea miaka 34 tangu kuanzishwa kwake. Kilele cha maadhimisho hayo, yalifanyika mjini Dodoma ambapo Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete, alizungumza na wananchi. Rais Kikwete, alizungumzia mambo mengi yanayohusu chama hicho na nchi yetu kwa ujumla. Hata hivyo si nia ya makala hii kujadili mambo yote aliyoyazungumza yakiwamo yale ambayo tayari yameonyesha kupokewa kwa maoni tofauti na wananchi wa kada mbalimbali kama ambavyo tumeona katika vyombo vya habari mbalimbali. Moja ya mambo yanayojadiliwa sana baada ya hotuba yake ni kauli yake kwamba yeye hawajui wamiliki wa Dowans na kwamba eti hata yeye hataki walipwe. Hilo tuliache. Lengo la makala hii ni kujadili eneo jingine kabisa katika hotuba hiyo nalo likiwa ni kupotea kwa taswira ya CCM na nia ya kufanywa mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya chama hicho. Kwanza nianze kwa kumpongeza kwa kuthubutu kuwaambia viongozi wenzake waliomwezsha kushinda uchaguzi mara mbili katika kipindi kizishozidi miaka mitano kwamba chama chao kimepoteza taswira nzuri na mvuto mbele ya umma na kwamba wengi wao ni lazima waondolewe ili kukijengea taswira mpya na bora zaidi. Mimi kama mwananchi wa kawaida kabisa ambaye ni mwanachama ninayeyumba kutokana na mikanganyiko mingi iliyojitokeza katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya utawala wake. Naweza kusema kuwa ni miongoni mwa watu waliofurahi kusikia kwamba kwa mara ya kwanza kiongozi wa juu kabisa wa chama amekuwa na mawazo ya kuchukua hatua za kuwawajibisha watendaji ambao wamekuwa mzigo kwa chama. Lakini ninatatizika kidogo kuelewa viongozi hao ambao uongozi wa juu una madaraka ya kuushughulikia ni upi? Maana tumekuwa na watendaji wengi ambao walikuwa wanasimamia zoezi la rushwa wakati wa kura za maoni ambao wanaanzia katika ngazi za matawi, kata wilaya hadi mkoa. Ni dhahiri viongozi waliohusika katika rushwa hawakuwa katika ngazi ya taifa ambako taratibu zake ziko wazi na zilizo katika mazingira ambayo huwezi kutoa rushwa kwa yoyote. Utampa rushwa Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti au Katibu mkuu utaanzaje? Katika ngazi hiyo, hupokewa matokeo ya kila jimbo na mapendekezo ya mikoa na wilaya tayari kwa uchambuzi wakati zoezi la rushwa likiwa limekwisha kufanyika katika ngazi hizo. Sasa Rais Kikwete anaposema viongozi watashughulikiwa ili kujenga taswira ndipo ninapojiuliza, viongozi gani? Wale walioajiriwa na CCM au wale wanaoteuliwa na mwenyekiti? Ukiangalia katika ngazi za wilaya na mkoa, kuna watendaji wengi ambao hufanya kazi za chama ambao hushiriki katika kupanga na kutoa maamuzi makubwa katika chama katika ngazi zao ambao naamini si mwenyekiti au mwingine yeyote anaweza kuwaondoa bila kutumia utaratibu wa nyakati za uchaguzi wa chama. Katika kundi hili, wapo wenyeviti, makatibu wa Itikadi na Uenezi, makatibu wa Uchumi na Fedha, wajumbe wa Halmashauri Kuu na wale wa Kamati za Siasa katika ngazi zote (tawi, kata, wilaya, mkoa hadi taifa). Binafsi najiuliza, hivi wakishughulikiwa wachache tu, tena wale walioajiriwa na chama, ndiyo taswira ya chama itajengeka upya? Hata hivyo mtizamo huu mimi unanipa tabu kidogo kwa maana naamini kwamba wananchi wa kawaida hawana jambo lolote wanalofanyiwa moja kwa moja na chama, linalowafanya wakichukie chama chao au kuharibu taswira. Binafsi naamini, chombo kinachoweza kuharibu taswira ya chama ni serikali kutokana na wananchi wanavyoweza kutokubaliana au kulalamika kwa jinsi serikali inavyochukua maamuzi mbali mbali ambayo wao wanaona yanawaumiza. Kwa mfano suala la Netgroup Solutions, Richmond, Dowans, EPA, uuzaji wa mabenki yetu kwa bei chee badala ya kuwaruhusu wawekezaji kuanzisha benki zao, mikataba ya madini, mishahara midogo, ugumu wa maisha unaotokana na uchumi wetu kuwa wa wasiwasi, gharama kubwa ya petroli kiasi cha wananchi kutojua EWURA ipo kwa sababu gani na wenzao wa TPDC. Kwa hakika, haya ndiyo yanayoharibu taswira ya chama chetu, bila kuyashughulikia haya hata ukifukuza watendaji wote wa ngazi ambazo una mamlaka ya kuwaondoa hakika taswira ya chama haiwezi kurudi. Wewe mwenyewe umeona baada ya hotuba yako ya Dodoma baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wasomi na wananchi wa kawaida walivyoonyesha kutokubaliana na suala moja tu ulilolitolea ufafanuzi la Dowans kwa kusema hata wewe hutaki walipwe na kwamba huwajui wamiliki wakati waziri wako akiwa tayari ameshawataja wale ambao wananchi wameshafanywa wasiamini kwamba ndio wenyewe kutokana na taarifa za kuchanganya wanazosoma kila siku katika vyombo vya habari. Wananchi wanaamini kuwa wahusika wa Dowans, wako ndani ya CCM, jambo linalopewa nguvu na baadhi ya mawaziri wako wanaotuhumu kwamba kuna baadhi wanataka kutengeneza fedha kwa ajili ya uchaguzi ujao wa urais. Ndiyo maana nakwambia, kutueleza taswira ya chama itajengwa kwa kuwaondoa viongozi walioajiriwa na chama tu huku serikali ikiendelea kuleta mikanganyiko isiyoleta majibu na kueleweka ndani ya uma, bila wakosaji kushughulikiwa ni kujidanganya. Binafsi naona wapo viongozi walioshiriki kuvuruga chama kwa nafasi zao ambao si wa kuajiriwa au walioko katika mamlaka yako ya uteuzi wakiachwa waeendelee kuvurunda, hapo ndipo ninaposema mzee wangu Kikwete mbali ya upendo wote nilionao kwako sijakuelewa. Tunataka kuona viongozi wote waliosababisha hali hii katika serikali yako wakiondoka au kuwajibishwa ili kujenga taswira nzuri ya chama. Mbona Lowasa, Karamagi na Msabaha na wengine wameondoka? Mzee Benjamin Mkapa kakuachia chama ukipata ushindi wa asilimia 80, zimepungua hadi asilimia 61, angalia usimuachie atakaye gombea katika uchaguzi ujao asilimia 30 kama hutacheza karata zako vizuri. Mabadiliko uliyoyasema yawe ya heri badala ya kuleta malalamiko makubwa na mkanganyiko ndani ya chama, vinginevyo vumilia hadi katika uchaguzi wa mwaka ujao wa chama. |
No comments:
Post a Comment