Mapya yaibuka Dowans • Dk. Slaa asema Kikwete anawajua wamiliki wake na Mwandishi wetu |
WAKATI kampuni ya kuzalisha umeme wa dharula ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd zikiwa zimewasilisha rasmi ombi la kuomba fidia ya sh bilioni 94 isajiliwe katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kulipwa sh bilioni 94, serikali imebakiza siku saba kuanza kuilipa kampuni hiyo kiasi hicho cha fedha. Hatua hiyo imetokana na serikali kusuasua kuweka pingamizi Mahakama Kuu dhidi ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC), iliyoipa ushindi Dowans katika kesi yake na Shirika la Umeme nchini (TANESCO). Kusuasua kwa hatua hiyo iliyolenga kuinusuru serikali kukwepa kulipa mabilioni hayo, kunapingana na dhamira ya Rais Jakaya Kikwete aliyelihutubia taifa siku ya kilele cha kumbukumbu ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma kwamba serikali kwa kutumia wanasheria waliobobea, inajiandaa kupinga hukumu hiyo mahakamani. Kikwete ambaye aliungana na kundi la Samuel Sitta, Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), kupinga kuilipa Dowans, aliwatia moyo Watanzania kuwa tayari wameshawaelekeza wanasheria kushirikiana na wale wa TANESCO kutafuta namna ya kukwepa kulipa kiasi hicho kikubwa cha fedha. Duru za kisiasa kutoka ndani ya Wizara ya Nishati na Madini, zililiambia gazeti hili kuwa pamoja na kauli na msimamo wa Rais Kikwete, hadi jana serikali ilikuwa haijawasilisha pingamizi la hukumu ya ICC, hatua ambayo inaweka mahali mabaya serikali kuanza kulipa sh bilioni 94 pamoja na riba ya sh milioni 17 kila siku kuanzia Februari 16. Mbali ya serikali kushindwa kuweka pingamizi hilo mahakamani hadi sasa, imebainika kuwa hata kundi la wana harakati lililotangaza awali kwenda mahakamani, halijafungua pingamizi hilo na badala yake limewasilisha mahakamani nia ya kutaka kuweka pingamizi dhidi ya Dowans. Habari hizo zilisema kuwa kesi hiyo imepewa namba 8/2011 na tayari imeshapangiwa Jaji wa kuisikiliza ingawa tarehe ya kuanza kusikilizwa bado haijapangwa. Hivi karibuni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salvatory Bongole, alisema ombi la Dowans dhidi ya TANESCO liliwasilishwa Januari 25 mwaka huu mahakamani hapo na wakili wa kujitegemea anayeiwakilisha kampuni hiyo, Kennedy Fungamtama. Kwa mujibu wa habari hizo, Shirika la Umeme nchini (TANESCO), limeiandika barua Wizara ya Nishati na Madini kutaka isaidie kulipa deni hilo baada ya kubaini kuwa hakuna uwezekano wa serikali kushinda au kupunguziwa malipo ya sh bilioni 94. “Hadi leo, tumebakiza siku saba tu kuanza kuilipa Dowans sh bilioni 94 na tayari TANESCO ilishapata notisi ya siku 21 ambazo zinaishia Februari 15. Ikifika tarehe 16 mwezi huu, tutaanza kulipa na fidia ya sh milioni 17 kwa kila siku. Hofu ya serikali kuanza kuilipa Dowans, ilielezwa jana na Mbunge wa Bumburi, January Makamba, aliyetaka serikali itoe maelezo lini itawasilisha pingamizi hilo mahakamani kwa hofu ya kubanwa kulipa riba ya sh milioni 17 kila siku. Tuzo hiyo ya Dowans iliamriwa na ICC Novemba 15 mwaka jana baada ya kampuni hiyo kuishinda TANESCO katika kesi yake ya kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba iliyokuwa imefunguliwa rasmi Novemba 20 mwaka 2008 na kupewa namba 15947/VRO. Tangu ICC itoe hukumu ambayo iliipa ushindi Dowans baadhi ya wananchi, wanasiasa wakiwemo na mawaziri na hata majuzi Rais Kikwete, walijitokeza hadharani kuitaka serikali isilipe fidia hiyo kwa madai kuwa kuilipa ni sawa na kuwazawadia mafisadi waliolidanganya taifa tangu ilipoletwa kwa kampuni dada ya Richmond. Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa Rais Kikwete anawajua Dowans na kamwe hawezi kujitenga na kampuni hiyo. Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia ya simu, Dk. Slaa alisema kuwa Rais Kikwete ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na maamuzi ya uwekezaji wa kampuni hiyo, yalipitishwa na baraza hilo. “Rais ana maswali mengi ya kujibu. Kama hawajui Dowans, atuambie nani anahusika nayo? Je, hakuhusika kupitisha azimio la mawaziri wake la kuiruhusu Dowans kuwekeza nchini?” alisema Dk. Slaa na kusisitiza kuwa Rais hawezi kuikwepa Dowans. |
No comments:
Post a Comment